Mambo muhimu ambayo yanatakiwa kuzingatiwa unapokuwa kwenye mahusiano

UKWELI ni kuwa watu wawili wanapoamua kwa dhati kuwa katika mahusiano ni kwamba wanakuwa tayari katika akili zao wamejenga matarajio au matumaini ya kunufaika na uhusiano husika.

Kunapokuwa na upendo, basi pia kunaleta majukumu, ambapo bila ya kutimizwa kwa majukumu yanayotarajiwa kutimizwa, maana halisi ya mahusiano bora inapotea.

Ni wazi kuwa mara nyingi majukumu yanayoletwa na upendo huwa hayaelezwi wazi wazi, hata hivyo katika mahusiano, mambo yafuatayo yanaweza kuwa sehemu ya matarajio ambayo wapenzi wanaweza kuwa makini ili waweze kuwapendeza wenzao.

Kwa maana nyingine ni kuwa yafuatayo, ndio maeneo ambayo mtu aliye kwenye mahusiano ni muhimu ‘acheze’ vema ili kulinda mahusiano au mapenzi yake.


Fedha

Katika suala la fedha, jambo kubwa linalojitokeza ni namna ya kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya fedha.

Ni muhimu kuweka mikakati ya pamoja kwa mambo ya msingi kimaisha na kila mmoja kutilia maanani mipango hiyo, kabla ya kuamua kutumia kipato chake kwa mambo ambayo pengine hayapo nje ya mipango ya kifedha ya wawili nyie kama wapenzi.

Bila shaka, kuendana na aina yenu ya kipato, aina yenu ya maisha, kama wapenzi mtakuwa na kiwango fulani cha fedha ambacho si busara mmoja wenu kuamua kutumia bila kumtaarifu mwenzake , hata kama matumizi husika ni muhimu sana na haijalishi nani kazitafuta fedha husika.

Imani
Katika suala la imani ni muhimu kufahamiana vema mwenendo wa kiimani wa mwenza wakona kuheshimu kuwa jambo hili ni nyeti.

Imani inaweza athiri namna mnavyoweza kuwasiliana kama wapenzi kwa sababu mwingine mwenye msimamo mkali wa kidini, anaweza kukataa jambo fulani hapo baadaye jambo ambalo pengine mwenza wake anaona ni jambo la kawaida tu.

Imani inaathiri malezi ya watoto na inaweza athiri shughuli za kiuchumi za wawili nyie, mfano pale mmoja wenu anapoamua kujikita katika ‘huduma’ zaidi kuliko familia na shughuli za kuingiza kipato.

Mahali pa kuishi

Mtaa gani , wilaya gani, mkoani gani, nchi gani au bara gani kila mmoja wenu anatazamia muishi ni jambo la msingi kuliweka wazi kati yenu.

 Jambo hili linaweza kuendana na mambo mengine mengi ambayo yanachochea mabadiliko ya muda mfupi na hata muda mrefu katika maisha yenu, kama vile , aina ya kazi mnazotarajia kila mmoja wenu kufanya, na aina ya kazi unazotamani au kufikiri ni vema mwenza wako afanye.

Watoto
Hili ni jambo zito haswa katika vipengele vya lini watoto wapatikane (ujauzito), idadi ya watoto, aina ya malezi kwa watoto watakaopatikana, na zaidi sana majukumu ya kifedha katika malezi ya watoto.

Pamoja na kutafakari hayo, watu wawili mlio katika mahusiano ni muhimu mkatengeneza picha ya maisha ya watoto wenu endapo mmoja wenu atatangulia mbele za haki na hata ikiwezekana mwaweza fikiria na kupanga aina ya maisha mnayotaka watoto wenu waishi pale nyote wawili hamtokuwapo duniani.

Inapotokea mambo kama hayo yaliyotajwa hapo juu hayajawekwa wazi mbele yenu ni rahisi mmoja wenu kufanya mambo yasiyompendeza mwengine.

Falsafa ya maisha
Suala hili linahusu wa kipekee na tafakari huru ya kila mmoja wenu kuhusu mambo kadhaa ya kimaisha kama vile mtazamo wa kila mmoja wenu kuhusu biashara.

Falsafa pia inahusu namna kila mmoja wenu anavyochukulia mambo kama vile kusaidia watu wengine, kuwa na mahusiano na watu wa jinsia tofauti .

Falsafa pia inahusika na namna kila mmoja anavyotafsiri mafanikio katika maisha, na alivyo tayari kufanya yanayopaswa kufanywa kufikia mafanikio.

Katika juhudi za kufikia mafanikio unawea kukuta wapenzi mnatofautiana kwani mmoja anaweza amini rushwa ndio suluhisho pekee la kufikia anakotaka, wakati mwingine anaamini tofauti na hivyo.

Hisia za kimapenzi

Ni jambo la msingi kutokupuuzia hisia za kimapenzi za kila mmoja wenu. Tambua vile mwenzako angependa akuone unamvutia na vile ambavyo unamjali hisia zake.

Ni kweli kuwa katika mahusiano, hisia za kimapenzi zinaweza zisichukue nafasi kubwa kati yenu kwani kuna mambo mengi ya kufanya pamoja kama wapenzi, hata hivyo pamoja na udogo wake wa muda, jambo hili nyeti lisipopewa kipaumbele, linaweza sababisha mengine yote kuharibika.

 Zaidi sana, kumbuka wewe na mpenzi wako, ni watu wa jinsia mbili tofauti, kinachowafanya muungane kiasili ni hizo hisia za mapenzi kati yenu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *