Faida za kufanya kazi kwa bidii

1. Utaweza kutumia muda vyema

Huwezi kutumia muda vyema kama hutofanya kazi kwa bidii. Ukiwa na bidii katika kufanya kazi, unaweza kufanya kazi za siku nzima ndani ya saa moja au kazi za siku mbili ndani ya siku moja.

Hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa bila kutumia muda vyema; muda ni mali, hivyo yakupasa uutumie vyema kwa kufanya kazi kwa bidii.

 

2. Kufikia malengo yako

Kanuni moja wapo ya kufikia malengo ni kufanya kazi kwa bidii. Safari ya mafanikio siyo ya mteremko, inahitaji juhudi nyingi ili tuweze kuona matokeo.

Hakuna mtu aliyewahi kufanikiwa kwa kufanya kazi kivivu; fuatilia watu waliofanikiwa watakueleza jinsi wanavyofanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ndoto zao.

 

3. Kuheshimika

Nani atamheshimu mvivu? Kwa hakika hakuna. Mtu anapokuwa mwenye bidii utasikia kauli kama vile huyo hapendi mchezo, akishaingia kwenye kazi zake humpati, hageukagi nyuma kwenye kazi huyo, kama huyo yupo hiyo kazi lazima iishe, n.k.

Hizi ni baadhi ya kauli zinazoonyesha kuheshimiwa kwa mtu husika kutokana na kufanya kazi kwa bidii. Ikiwa unataka kuheshimika ni lazima ufanye kazi kwa bidii.

4. Kutambulika

Ikiwa unafanya kazi kwa bidii huna haja ya kujikombakomba kwa wakubwa au mbele za watu ili utambulike; bidii yako ya kazi itakutambulisha.

Naamini umewahi kusikia watu wakipewa tuzo kwenye sherehe za kitaifa kutokana na kufanya kazi kwa bidii; hili linatupa picha ya kipekee ya faida ya kufanya kazi kwabidii.

Usijali hata kama wanakudharau au wanakuona duni, wewe fanya kazi kwa bidii watakutambua ukiwepo au hata wakati utakapoondoka wataona pengo lako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *