Sakata la vigogo wa CCM kuhojiwa ripoti kukabidhiwa wiki hii

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Dk. Ally Bashiru amesema ripoti ya mahojiano na Makatibu wakuu wastaafu Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe itakabidhiwa wiki hii kwa kamati ndogo ya nidhamu.

Ilielezwa baada ya kupokelewa na kamati hiyo itapelekwa kwa kamati kuu ya chama na hatima yao kujulikana kabla ya marchi 1, 2020.

Hivi karibuni Kamati Kuu ilitoa siku saba kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama hao watatu na kuiwasilisha katika vikao husika.

Kamati Kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli ilikaa Jijini Dar es Salaam na kuamua hatma ya vigogo itajulikana baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula, kuwasilisha taarifa zao ndani ya siku saba.

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, ilieleza kuwa, kamati kuu iliazimia kuwa taarifa zao kuwasilishwa katika vikao husika.

“Kamati Kuu imetoa siku saba kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama hawa watatu na kuiwasilisha katika vikao husika,” alisema Polepole.

Alisema kamati hiyo ilipokea taarifa ya awali kutoka kwa Kamati ya Usalama na Maadili juu ya Utekelezaji wa Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) katika Kikao chake cha Desemba mwaka jana Jijini Mwanza, kuhusu kuwaita na kuwahoji wanachama hao.

Vigogo hao waliitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya baada ya sauti zao kuenea katika mitandao ya kijamii.

Viongozi hao wastaafu walikuwa wakielezea namna CCM inavyopoteza mvuto, uendeshaji wa nchi na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mtu anayewachafua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *