Hatma ya Halima Mdee kufahamika Aprili Mosi

Mbunge wa Chadema jimbo la Kawe Halima Mdee anakabiliwa na shtaka la kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli ambapo alifikishwa katika mahakama ya kisutu kwa mara ya kwanza Julai 10, 2017.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa, ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.

Katika kesi hiyo ambayo imechukua takribani miaka miwili sasa leo Februari 20 upande wa mashtaka umefunga ushahidi baada kujiridhisha na mashahidi watatu waliotoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa amesema shauri lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini kwa upande wao wameridhika na mashahidi watatu waliotoa ushahidi mahakamani hapo.

“Shauri lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini upande wetu wa Serikali tumeridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wetu watatu hivyo tunafunga ushahidi,”alidai Simon.

Baada ya maelezo hayo upande wa Utetezi, Hekima Mwasipu aliiomba mahakama hiyo ndani ya siku 14 kuwasilisha hoja kwa njia ya maandishi kama mteja wao ana kesi ya kujibu au la.

Upande wa mashtaka utawasilisha hoja zao siku 14 baada ya kupokea hoja zao za upande wa utetezi .

Hakimu Simba alisema Machi 6, 2020 upande wa utetezi utawasilisha hoja zao na Machi 20, 2020 upande wa mashtaka utawasilisha majibu ya hoja za upande wa utetezi.

Shauri hilo litarudi tena Aprili Mosi, 2020 kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *