Wanafunzi waandamana kwa RC kupinga adhabu zilizokithiri shuleni


Wanafunzi wanaosoma shule ya Sekondari Shinyanga (SHYBUSH), iliyopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, wameandamana kwenda kwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack wakilalamika kunyanyaswa na walimu, pamoja na kupewa adhabu zilizokithiri shuleni hapo.

Akizungumza jana kwa niaba ya wanafunzi wenzake Kaka mkuu wa shule hiyo Mwendesha Manyangu mara baada ya kufika kwa mkuu wa mkoa, alisema kumekuwa na malalamiko mengi ya wanafunzi kunyanyaswa na walimu shuleni hapo, pamoja na kupewa adhabu kwa makosa ambayo wangeonywa.

Alisema baada ya kilio hicho kuwa cha muda mrefu huku wakimweleza matatizo yao mkuu wa shule hiyo Malambi Malelemba amekuwa hawajali, ndipo wakaamua kuandamana kwenda kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kupaza kilio chao ilikupatiwa ufumbuzi.

“Tumeamua kuandamana kuja kumuona mkuu wa mkoa, tukiamini atatusikiliza matatizo yetu yanayotukabili shuleni na kututatulia, ikiwamo kupewa adhabu zilizokithiri, kwasababu tumechoka na manyanyaso ya walimu hatu somi kwa raha,”alisema Manyangu.

Naye Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, aliwatoa wasiwasi wanafunzi hao na kubainisha kuwa malalamiko yao atayafanyia kazi, huku akiwa waonya kuacha kujiingiza kwenye migomo isiyo na maana ambayo inawapotezea muda wa masomo.

Pia aliwaonya wanafunzi ambao wamekuwa wahamasisha migomo shuleni, waache tabia hiyo mara moja, na kubainisha wale ambao wamehamasisha maandamano hayo watashughulikia ili liwe fundisho kwa wanafunzi wengine

Aidha Kaimu Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Joseph Paul, aliwataka wanafunzi kuachana na makundi ambayo hayawajengi na kuanzisha migomo isiyo na faida, huku akishukuru hawakufanya fujo shuleni kwao ya kuharibu mali, na kuwasihi pale wanapokuwa na matatizo wafuate utaratibu.

Alipotafutwa kwa njiabya simu mkuu wa shule hiyo hakupokea simu na alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *