TMA yatoa tahadhari ya mvua kubwa katika mikoa 17


MVUA kubwa zinatarajia kunyesha ndani ya kipindi cha siku tano kuanzia jana kwenye mikoa 17 ikiwemo mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Kwa mujibu wa utabiri wa siku tano uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mvua hizo zimeanza jana kwa baadhi ha maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na zitaendelea katika mikoa ya Katavi, Kigoma, Tabora, Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu na Shinyanga.

Meneja wa Huduma za Utabiri wa TMA, Samuel Mbuya, alisema kwa siku ya kesho mvua kubwa zinatarajiwa katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Songwe, Iringa na Njombe.

“Athari zinazoweza kutokea ni kubwa hususani kwa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam ambapo kunaweza kutokea kwa uharibifu wa miundo mbinu, maeneo ha makazi kuzungukwa na maji na hali mbaya zaidi kwa wakazi wa maeneo ya mabondeni,” alisema Mbuya.

Alisema hali ya maeneo ya makazi kuzungukwa na maji pia inatarajiwa kwa mikoa mingine iliyotajwa na hivyo shughuri za kiuchumi uwenda zikasimama.

Mbuya, alisema kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa zaidi kutokana na kuwepo kwa dalili ya vimbunga pacha katika bahari ya Hindi.

“Kuna mgandamizo mdogo wa hewa unaoendelea kuimarika vinavyotarajia kutengeneza vimbunga pacha magharibi mwa bahari ya Hindi na kuathiri mifumo ya hali ya hewa,” alisema Mbuya.

Aliongeza kubwa vimbunga hivyo vinaonekana katika Pwani ya Somalia na Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Madagascar na kusababisha ongezeko la mvua kubwa katika Pwani ya kaskazini ya nchi yetu katika siku ya jana na leo.

Kutokana na matarajio hayo, TMA imetoa tahadhari kwa wananchi na Mamlaka husika juu ya athari zinazoweza kutokea na kuwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa wanazozitoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *