Marufuku kufungia biashara zinazodaiwa kodi

Serikali imepiga marufuku mamlaka zinazohusika kusimamia biashara kwa namna tofauti, kutofunga kiwanda chochote ambacho kitabainika  kwenda kinyume cha utaratibu ikiwemo ukwepaji wa kodi.
Marufuku hiyo imetolewa na Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mara baada ya kuwasili mkoani humo kwaajili ya kufanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali iliyopo chini ya Wizara yake.
Naibu Waziri huyo amesema badala ya kufunga viwanda mamlaka hizo zinatakiwa kuwekeza nguvu nyingi katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa ulipaji wa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya nchi na sio kutumia nguvu.
Amesema kuwa kwa muda mrefu mamlaka hizo zimekuwa zikitoa adhabu kali kwa lengo la kukomoa badala ya kufundisha.
“Tumetengeza njia mbaya sana ya kukusanya  kodi  yaani unakwenda kule unamnyanyasa mwekezaji badala ya kwenda kirafiki mzungumze na muelewane kuanzia leo nasema ni marufuku kufungia kiwanda kisa tu kinadaiwa kodi na makosa kama hayo” amesema Manyanya.
Amesema kuwa vitendo vya kufungia viwanda kama adhabu vimekuwa vikiwaumiza wafanyabiashara ambao wamewekeza kiasi kikubwa cha fedha, hivyo kuwafungia ni kuwavunja moyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *