Tanzania watu zaidi 1.2 milioni wanatumia ARV, Vijana wameathirika zaidi

Serikali ya Tanzania imefanikiwa kutoa bure dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) kwa watu zaidi ya 1.2 milioni huku kundi la vijana likitajwa kuwa limeathirika na ugonjwa huo ambao mpaka sasa tiba yake haijapatikana.
Idadi hiyo ya wanaotumia ARV ni asilimia 98 ya zaidi ya watu 1.4 milioni waliopima na kufahamu hali zao waliopimwa katika kampeni ya Kimataifa ya mapambano dhidi ya Ukimwi.
Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk James Kamuga amesema zaidi ya watu 1.6 milioni wanakadiriwa kuishi na VVU.
 “Watu zaudi ya milioni moja wamefanikiwa kupunguza makali ya VVU kupitia mpango na kampeni mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi”.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na VVU, Leticia Kapela ameishukuru Serikali kwa kutoa bure dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi na hivyo kuwezesha watu wasio na uwezo kiuchumi kupata dawa.
“Watu wengi wanaoishi na virusi vya Ukimwi, hasa kutoka familia maskini wangekufa mapema iwapo Serikali isingetoa bure dawa za kupunguza makali ya virusi,” amesema Leticia
Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TacAIDS), Dk Leonard Maboko amesema maambukizi mapya ya Ukimwi yameshuka kutoka zaidi ya watu 100,000 kwa mwaka kipindi cha miaka 10 iliyopita hadi kufikia zaidi ya watu 72,000 mwaka 2016/17.
Mkurugenzi mkazi wa UNAIDS Leo Zekeng, amesema zaidi ya watu 38 milioni waligundulika kuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi duniani huku kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 likiwa limeathirika zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *