TPA imetenga Sh bilioni 1.1 kujenga barabara na soko la kisasa

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Ziwa Tanganyika, imetenga Sh. bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na soko litakalohudumia watumiaji wa bandari ya Kagunga iliyopo mpakani mwa Tanzania na Burundi.

Kati ya fedha hizo Sh. milioni 930 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha changarawe inayounganisha mpaka wa Burundi kuelekea katika bandari hiyo na Sh. milioni 190 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa lililopo karibu na bandari hiyo.

Meneja wa Bandari ya Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese, ameelezea miradi hiyo mbele ya waandishi wa habari waliotembelea bandari hiyo kwa ajili ya kuona miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TPA katika ziwa hilo ikiwamo ya ujenzi wa magati ya kisasa.

“Ukija katika bandari hii utashuhudia barabara ya kiwango cha lami ambayo imeishia katika mpaka wa Burundi hivyo barabara ya kuingia bandarini haijaunganishwa ndio sababu TPA ikatenga Sh. milioni 930 kwa ajili ya kulipa fidia za wakazi wa eneo litakapopita mradi na kujenga barabara ya kiwango cha changarawe yenye urefu wa mita 700,” amesema Msese.

Amesema lengo la kushirikiana na Halmashuari ya Wilaya hiyo kufanya mradi wa ujenzi wa soko ni kufungua fursa za kibiashara katika bandari hiyo inayounganisha nchi za Tanzania, Burundi, Zambia na Congo.

“Ni sehemu ya kimkakati kuwa na bandari hii, hivyo ni muhimu kuwa na mazingira mazuri kama miundombuni imara ili kuunganisha nchi hizo tatu kibishara hasa kupitia soko hili tunalojenga,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *