Kesi ya Malinzi:Shahidi adai fedha za wadhamini zilizotolewa na TBL zilitumika bila nyaraka

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Richard Magongo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu fedha za wadhamini zilizotolewa na TBL kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kudhamini timu ya Taifa zilitumika bila kuwa na nyaraka za uthibitisho wa matumizi.

Magongo ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Benki ya Barclays alidai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, katika kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake.

Akiongozwa na Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, shahidi huyo alidai Mei 2012 kampuni ya TBL iliingia mkataba na TFF kwa aojili ya udhamini wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa kipindi cha miaka mitano.

Alidai kuwa kila mwaka kampuni hiyo ilikuwa ikitoa Dola za Marekani milioni mbili kila baada ya robo mwaka kwa kipindi cha miaka mitano hivyo jumla ni Dola za Marekani milioni 10.

Shahidi huyo alidai katika masharti ya TBL iliitaka TFF kuleta hesabu ya kila robo mwaka kabla ya kupewa fedha nyingine na kutaka nyaraka za kudhibitisha matumizi.

Pia alidai walianza kukagua matumizi ya mwaka 2013 na mara ya mwisho walifanya ukaguzi wa robo ya mwisho ya mwaka 2017 na kudai aliwajibika kufanya ukaguzi.

Shahidi huyo alidai baada ya kupitia ripoti hiyo waligundua fedha za wadhamini zizotumika zilikuwa hazina nyaraka za kutosha kudhibitisha uhalali wa matumizi.

Pia alidai matumizi mengine hayakuwa ndani ya mkataba wa TBL na TFF pamoja na mapungufu ya kihasibu na kiutawala wa TFF katika utekelezaji wa mkataba.

Alidai walibaini malipo yaliyokuwa yamelipwa kwenda kwa Jamali Malinzi ambapo kulikuwa hakuna udhibitisho kama mkopo umetolewa lakini kwenye ripoti ilionyeshwa yeye kulipwa.

Alidai miongoni mwa matumizi ambayo hayakuwa na nyaraka ni ya Dola za marekani 902,981.81 ya Mei 8,2014.

Hakimu Maira aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 20 mwaka huu itakapoendelea na usikilizwaji.

Mbali na Malinzi washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Meneja wa Ofisi TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017.

Miongoni mwa mashitaka hayo ni kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola za Marekani 173,335.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa sababu wanakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *